Idara hiyo imewataka watu hao ambao wamekuwa wakikimbia msako maalumu unaofanywa na idara hiyo kwa kushirikiana na idara ya kazi wenye lengo la kuwabaini wageni wanaoishi na kufanya kazi hapa nchini kinyume na taratibu kujisalimisha mara moja.
Akizungumza ofisini kwake leo afisa wa idara ya uhamiaji mkoani Kagera, Abdallah Towo ambaye ni kamishina msaidizi mwandamizi amesema msako ni endelevu hivyo katika kipindi hicho kilichotolewa kwa wale wote waliojificha wajitokeze kabla ya kufanyika shughuli ya kuwasaka itakayovihusisha vyombo vyote vya dola.
Afisa huyo amesema kwa mwezi Januari idara hiyo ilifanya misako ya kushtukiza katika taasisi mbalimbali 15 na kuwabaini wageni 97 wanaofanya kazi katika taasisi hizo na kati yao watano walikutwa hawana vibali vya kufanya kazi na kuishi nchini.
Amesema idara hiyo pia iliwanasa wahamiaji haramu 92 ambao walifikishwa mahakamani na wengine kufukuzwa nchini huku wanaowaingiza nchini wakitozwa faini.
Kwa upande wake, afisa kazi mfawidhi katika mkoa wa Kagera, Samwel Mgila amewataka waajiri katika mkoa wa Kagera hasa wanaomiliki shule binafsi za sekondari na za msingi kufuata taratibu na kanuni katika suala zima la kutoa ajira kwa wageni toka nje ya nchi.
Mkoa wa Kagera ni moja ya mikoa inayokabiliwa na wimbi kubwa la wahamiaji haramu ambapo mkoa huo unakadiriwa kuwa na wahamiaji haramu zaidi ya 39,000 toka katika nchi mbalimbali zinazopakana na mkoa huo, huku wengi wao wakiishi maeneo ya vijijini.




