Tuesday , 8th Apr , 2014

Vijana nchini Tanzania wametakiwa kuwa makini na utandawazi kwani unaweza kuwa na athari katika malezi na hata ukuaji wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa huduma ya Voice of Hope Ministry, askofu Peter Mitimingi, akiwa katika moja ya huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.

Tahadhari hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa huduma ya Voice of Hope Ministry, askofu Peter Mitimingi, wakati wa kongamano la vijana juu ya umuhimu wa kutenda mambo yanayoendana na maadili ya Kitanzania.

Kongamano hilo limefanyika katika kanisa la City Christian Centre jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya vijana elfu tano kutoka imani zote za kidini walihudhuria na kujifunza namna ya kutunza maadili na kuachana na tabia pamoja na matendo potofu.

Askofu Mitimingi amefafanuwa kuwa vijana wamekuwa wakiharibika kitabia na kimalezi kutokana na kupanuka kwa utandawazi, hasa namna jamii na vijana hao wanavyoweza kupata taarifa ya yanayoendelea katika nchi nyingine ulimwenguni.

Askofu Mitimingi amesema utandawazi umesababisha vijana kuiga na kutenda mambo yasiyoendana na utamaduni wao, ambapo ametoa mfano jinsi vijana wanavyovaa mavazi ya aibu na kuiga tabia kama ngono za utotoni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.