Friday , 20th Nov , 2015

Uongozi wa klabu ya Yanga umelitaka chirikisho la soka nchini TFF kuangalia na kuweza kupanga vizuri ratiba kwa ajili ya ushiriki wa timu ya taifa katika mashindano mbalimbali ili kutoa nafasi wachezaji wengine wa vilabu kuendelea na mazoezi.

Katibu mkuu wa klabu ya Yanga Jonas Tiboroha amesema, kwa sasa wamebakiwa na wachezaji wachache kutokana na wachezaji wengi kuwa katika timu za Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes ambazo zinajiandaa na michuano ya Chalenji hivyo wanashindwa kuwaandaa vizuri wachezaji waliobakia kwa ajili ya michuano ya Afrika ambapo ni muda mchache uliobakia kwa ajili ya maandalizi.

Kwa upande wake, kocha msaidizi wa klabu ya Yanga Juma Mwambusi amesema, TFF inabidi ikae chini na kuangalia kwani kuna wachezaji ambao wanachaguliwa kuunda kikosi cha timu ya taifa lakini hawatumiki, hivyo wangewagawa na kuweza kupata kikosi ambacho kingeshiriki michuano ya kuwania kufuzu kombe la dunia ili kupata muda wa kupumzika na kikosi kingine kiweze kushiriki michuano ya Chalenji.

Mwambusi amesema, wachezaji wanatumika sana hivyo kama wangepanga vizuri kikosi hicho kila mchezaji angepata nafasi na muda mzuri wa kupumzika na kuweza kuwa na nguvu mpya kwa ajili ya kuitumikia klabu yake.