Friday , 20th Nov , 2015

Serikali kupitia idara ya madini mkoani Shinyanga, imefanikiwa kuutoa mwili wa Mussa Supana aliyefariki shimoni akiwa na wenzake watano ambao waliokolewa hivi karibuni wakiwa hai katika mashimo ya Nyangarata wilayani Kahama.

Mmoja wa Manusra hao akiendelea na matibabu.

Kaimu Kamishina wa madini wa Wizara ya Nishati na Madini, Ally Samaje, alisema mwili huo uliopolewa jana usiku kwa jitihada za wachimbaji na wataalamu kutoka wizara hiyo ambao walifanikiwa kuutoa ukiwa umeharibika.

Samaje alisema baada ya kuutoa mwili huo, maafisa wake wa madini wa wilaya ya Kahama kwa kushirikiana na uongozi wa mgodi uliowafukia wanashughulikia kuusafirisha mwili huo kwenda wilayani Magu mkoani Mwanza kwa ajili ya mazishi.

Supana akiwa na wenzake watano, Chacha Wambura, Amos Mhangwa, Msafiri Gerard, Joseph Bulule na Onyiwa Morisi walifunikwa na kifusi baada ya kuangukiwa na udongo Oktoba 5, mwaka huu, katika mgodi huo unaochimbwa kienyeji.

Novemba 15, mwaka huu, wachimbaji watano waliokolewa wakiwa hai baada ya kuishi ndani ya shimo hilo kwa siku 41, hivi sasa wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama hali zao zikiwa zinatengemaa.