Tuesday , 6th Oct , 2015

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania imekanusha uvumi wa kuwa kuna vyama vya siasa vimepitiliza gharama za kuendesha kampeni kinyume na sheria ya gharama ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Mwanasheria kutoka ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Ludovick Ringia

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mwanasheria kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa Ludovick Ringia amesema kuwa kwa mujibu wa sheria hadi sasa hakuna uthibitisho utakaoweza kusema kuwa kuna chama kimezidisha gharama mpaka hapo uchaguzi utakapo kamilika.

Rengia amesema kuwa endapo chama au mgombea takayebainika amepitiliza gharama hizo baada ya uchaguzi sheria itafuata mkondo wake ikiwa ni pamoja na kufunguliwa mashitaka ya kijinai pamoja na kuvuliwa wadhifa wake.

Aidha amesema sheria zitakazo sababisha mgombea huyo kuzuiliwa ikiwa no pamoja na kutokujaza fomu au kujaza fomu kwa kudanganya kwa sababu sheria inasema kila chama au mgombea ni lazima aandike gharama zake hata kama vifaa anavyotumia ni vya msaada.

Mwanasheria huyo amesisitiza kuwa sheria ya gharama za chaguzi hazilengi matumizi ya fedha peke yake bali na vifaa kama magari, chopa na vinginevyo lazima vyama viandike ni nani anagharamia na ni kwa kiasi gani gharama za mafuta zinaendesha vyombo hivyo.