Wazee Maarfu wakiwa kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia katika jimbo la Newala Vijijini mkoani Mtwara.
Chama cha Wastaafu na Wazee Mkoa wa Mtwara (CHAWAMU) kimelalamikia kitendo cha wanasiasa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi zote, kuwasahau wazee katika sera zao wanazozitoa wakati wa kuomba kura.
Akizungumza leo mkoani humo, katibu wa chama hicho, Wilbard Nandonde, amesema chama kinashangazwa na baadhi ya wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani kutoongelea juu ya mustakabali wa changamoto zinazowakabili wazee na badala yake wanajikita kutoa ahadi katika nyanja nyingine.
Kwa upande wake, mwanachama wa chama hicho, Erntrudis Mpokwa, ameitaka manispaa ya Mtwara Mikindani, kutoa msamaha wa kodi za majengo kwa wazee wastaafu wa manispaa hiyo, ambao uwezo wao wa kipato ni mdogo.
Chama hicho kimejipanga kuadhimisha siku ya wazee duniani itakayofanyika Oktoba 1 mwaka huu, katika wilaya ya Nanyumbu mkoani humo, ambapo kitaifa itaadhimishwa mkoani Kigoma.