Thursday , 17th Sep , 2015

Msanii nguli toka Nigeria 2Face Idibia amefunguka kuhusu historia ya maisha yake na kusema kuwa almanusura apoteze maisha akiwa na umri wa miaka 26 tu, kwa ajali ya gari ambayo ilisababishwa na ulevi wa pombe.

Msanii 2Face ametoa siri hiyo ikiwa ni moja ya vitu ambavyo vitakuwepo kwenye kitabu chake anachotarajia kukizindua siku ya kuzaliwa kwake tarehe 18 mwezi huu, ambacho kitaelezea maisha yake binafsi.

Akielezea tukio hilo msanii 2Face anasema " Nakumbuka ilikuwa Lagos, nikiendesha kutoka maeneo ya fukwe za Kurano na nilikuwa nimelewa..nilipofika eneo la kona....ghafla nikajikuta nimeamka nikiwa hospitali, na nikasema hivi ndivyo ambavyo ningeondoka... kama hivi, na baada ya ajali hiyo nikaanza kuwa muoga wa mwendo kasi".

Nguli huyo wa kibao cha African queen anatarajia kuzindua kitabu chenye wasifu wake alichokipa jina la A very Good Bad Guy, siku ya ijumaa wiki hii, ambacho kitakuwa na historia yake, mahojiano yake na watu mbali mbali, maoni na michango ya watu mbali mbali waliokuwa na mchango mkubwa kwake, mashairi pamoja na nyimbo zake.