Tuesday , 15th Sep , 2015

Serikali ijayo imetakiwa kuelekeza rasilimali za nchi katika nafasi za ajira zilizopo, ili kuweza kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana, kwani kuna uhitaji mkubwa wa rasilimali watu katika sekta mbali mbali hapa nchini.

Rai hiyo imetolewa na na Dokta George Kahangwa ambae ni Mhadhiri wa chuo Kikuu cha Dar es salaam, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super mix kinachorushwa na East Africa Radio.

Dkt. Kahangwa amesema endapo rasilimali za nchi zikielekezwa kwenye ajira, tutakabiliana na tatizo la ajira kwa kuajiri watu na kupeleka utolewaji wa huduma bora.

" Serikali ijayo ina mambo kadhaa ya kufanya, moja wapo ni kulekeza rasilimali za nchi katika nafasi zile za ajira ambazo zipo lakini bado hazijajazwa, tuna uhitaji mkubwa wa walimu, madaktari na watu katika sekta mbali mbali zilizopo katika nchi yetu, kwa hiyo zikielekezwa kule ziajiri watu wa kutosha tuondokane na lile tatizo la watu kutotosha katika sekta mbali mbali," alisema Dkt. Kahangwa.

Pamoja na hayo Dkt. Kahangwa amesema pia serikali inatakiwa kupanua uchumi kwa sekta ambazo zinaibuka kama zile za gesi na mafuta, kwani itasaidia kukuza ajira na kuweza kuajiri vijana wengi hapa nchini, na pia serikali kuishirikisha jamii katika utoaji wa huduma mbali mbali.

Akiongelea suala la Elimu ambalo amesema ni changamoto kubwa kwa vijana, Dkt. Kahangwa amesema vijana wanatakiwa kuwa wabunifu ili waweze kutengeneza ajira na kuajiri Watanzania wengine, pamoja kuwa na uzalendo wa kuthamini bidhaa zinazotengenezwa hapa nyumbani, ili kuweza kutatua soko la bidhaa za hapa nchini.

"Tunayo elimu ambayo haijaelekeza sana kama aliyepata elimu hiyo anaajirika au ajiajiri mwenyewe, hivyo kuwe na ubunifu ambao utaweza kutengeneza ajira na kuajiri wengine, haya ni mambo ya kuyafanyia kazi," alisema Dkt. Kahangwa.

Pia Dkt. kahangwa amesisitizia suala la kufufua viwanda, na pia viwe na uwezo wa kutengeneza bidhaa zenye ubora zitakazoweza kununulika hata kwa nchi nyingine.