Kaimu Mganga mkuu wa manispaa ya Morogoro Dkt. Said Mbwana
Kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Morogoro Dkt. Said Mbwana amesema tangu kulipuka kwa ugonjwa huo mwanzoni kwa agosti mwaka huu,jumla ya watu 93 waliugua ugonjwa huo na kufikishwa kwenye kambi maalum iliyoanzishwa katika hospitali ya sabasaba,na wote walifanyiwa matibabu na kuruhusiwa.
Aidha Dkt. Mbwana ameongeza kuwa kwa sasa wanasubiri wiki mbili zijazo kama hakutotokea maambukizi mengine mapya watafunga kabisa kambi hiyo na kwamba walijipanga kwa mikakati mbalimbali ikiwemo usafi, elimu na madawa ya uhakika kwa wakati kukabiliana na hali hiyo.
Nao wafanyabiashara wa vyakula maarufu kama mama lishe mbali na kulalamikia kutokufanya biashara kwa kipindi kirefu kwa kukimbizwa na askari wa manispaa na maafisa afya, wameeleza kufurahishwa na kuondoka kwa ugonjwa huo sambamba na kutoa wito kwa wenzao kuzidi kuimarisha hali ya usafi na kuzingatia matumizi ya maji safi ili kudhibiti mlipuko mpya wa ugonjwa huo.
Kwa upande wake wananchi wameuomba uongozi wa manispaa hiyo kuacha kukaa maofisini baada ya ugonjwa huo kwisha badala yake waendelee kutoa elimu ya usafi mitaani badala ya kusubiri matatizo.
Mtu mmoja mkàzi wa Kilakala alipoteza maisha mara baada ya kuibuka kwa ugonjwa huo, huku changamoto kubwa ya kuenea kwa ugonjwa huo ikitajwa kuwa ni uchafu na matumizi ya maji yasiyo salama kutoka vyanzo visivyo aminika ikiwemo mtoni.

