Friday , 11th Sep , 2015

Kikosi cha jeshi la kujenga Taifa cha mgambo JKT 835 kilichopo Kabuku Wilayani Handeni kinatarajia kuingiza mbegu mpya ya mahindi ya TMV1 sokoni tani 100 ikwa ni mikakati yake ya kukabiliana na baa la njaa nchini.

Baadhi ya wanakikosi cha jeshi la kujenga Taifa cha mgambo JKT 835 kilichopo Kabuku Wilayani Handeni

Mkuu wa kikosi hicho Meja Rashidy Kanole ameyasema hayo wakati wa sherehe ya kumaliza mafunzo ya awali ya kijeshi kwa mujibu wa sheria "Operesheni Kikwete" kuwa mbegu hizo zinazalishwa kupitia kampuni mpya iliyosajiliwa na jeshi la kujenga taifa JKT ya Seed Company ltd.

Meja Kanole alisema mbegu hiyo itatoka kwenye ekari 100 walizolima mwaka huu na kwamba mbegu hiyo wataisimamia ipasavyo sokoni ili kuondokana na uchakachuaji unaoweza kufanywa na wafanyabiashara wengine na kuongeza kuwa wataweka wazi mahali mbegu hiyo itakapopatikana.

Sambamba na hayo ameongeza kuwa katika kufikia malengo hayo wamepanda miche elfu 20 ya michungwa katika eneo la Songa na kueleza kuwa bado wanaendelea kufikia ndoto yao ya kuzitumia ekari 2000 zilizoko Songa zijae michungwa.

Akitoa salamu za mwakilishi wa Jeshi la Kujenga Taifa, mkurugenzi wa operesheni na mafunzo JKT Luteni Kanali Abubakary Charo amewataka wahitimu hao kuyatumia mafunzo hayo waliyoyapata ya uadilifu kwa kama sehemu ya kuandaa kizazi kijacho chenye uwezo wa kupinga rushwa kwa maslahi ya ustawi wa taifa.

Luteni Kanali Charo amesema kuwa mafunzo waliyoyapata wahitimu hao yatawasaidia kuibadilisha jamii kutoka katika mtazamo hasi na kuingia katika mtazamo chanya ikiwa ni pamoja na kufuata maadili ya kazi yao yanavyowaongoza kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.

Jumla ya vijana 1507 wa mujibu wa sheria wamehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambayo yalichukua takribani miezi mitatu tangu walipoanza rasmi mafunzo yao.