Thursday , 10th Sep , 2015

Wazazi wametakiwa kuwaandaa watoto wao kwa elimu ya sekondari mara baada ya kumaliza mitihani yao ya elimu ya msingi inayoendelea hivi sasa nchini kote, na si kuwaacha nyumbani.

Wito huo umetolewa na mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mzimuni iliyopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam, Bi. Debora Mbaga, alipokuwa akiongea kwa njia ya simu kwenye kipindi cha Super mix kinachorushwa na East Africa radio.

Mwl. Mbaga amesema wazazi wanatakiwa watambue kuwa kuhitimu elimu ya msingi kwa watoto hao sio sababu ya kuwaacha nyumbani bila shughuli yoyote, bali wawaandae watoto kwa masomo ya awali ya elimu ya sekondari, ili watakapoingia sekondari wawe na uzoefu.

Mwl. Mbaga pia amesema kwa kufanya hivyo kutawaepusha watoto na kujiingiza kwenye makundi ambayo yatawaharibu kitabia, na pia kuongeza elimu yao, kwani wao kama walimu wanatarajia watoto hao watafanya vizuri na kuendelea na elimu ya sekondari.