Rais wa ZFA ambaye anamaliza muda wake leo Ravia Idarous Faina akiwa mbele ya wajumbe
Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya (ZFA) Afan Othman, amesema mkutano wa uchaguzi utafanyika katika uwanja wa michezo wa Gombani Chake chake Pemba ambapo mkutano huo unatarajiwa kumchagua Rais wa ZFA Taifa na Makamu wake wawili kwa mujibu wa Katiba ya ZFA ambao mmoja atafanya kazi zake Unguja na mwengine Pemba ambapo watu saba wamejitokeza kugombea nafasi hizo.
Afan aliwataja wagombea waliopitishwa na Kamati yake kuwania nafasi hizo kuwa ni pamoja na Rais wa sasa wa chama hicho Ravia Idarous Faina anaeshindana na aliewahi kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Salum Bausi Nassor, wanaowania urais wa ZFA wakati aliewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Mzee Zam Ali akiwania nafasi ya Makamu wa Rais wa ZFA Taifa Unguja.
Katika kinyang’anyiro hicho, Zam atakabiliwa na upinzani mkali toka kwa Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Malindi Mohamed Masoud na Mtoto wa mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa stars Nassor Mkweche, Salum Nassor Mkweche wakati Makamu wa Rais wa ZFA Pemba wa sasa, Ali Mohammed Ali anakabiliana na Hamad Sued.
Afan amesema wajumbe 57 wa mkutano mkuu huo kutoka katika vyama vya soka vya wilaya zote za Zanzibar na wajumbe kutoka katika Kamati mbalimbali za chama hicho wameshapewa taarifa na wanatarajiwa kupiga kura huku akiwahakikishia wapenda soka kuwa watajitahidi kutenda haki kwa kutumia Katiba na kanuni za uchaguzi huo.
Afan amesema hadi asubuhi ya jana maandalizi yote muhimu yalikuwa yamekamilika ikiwemo kuwasili kwa wajumbe wa kamati yake pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu kutoka Unguja huku vifaa vyote muhimu vikiwa vipo tayari.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuhudhuria pia na Mjumbe kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na mwakilishi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) unatarajiwa kuhitimisha mzozo wa muda mrefu wa uongozi ndani ya chama hicho uliopelekea kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura mwezi Februari mwaka huu ulioamua kumfukuza uongozi na kumfungia kutoshiriki katika shughuli za mpira wa miguu kwa muda wa miaka minne aliyekuwa Makamu wa Rais wa ZFA Unguja Haji Ameir Haji baada ya kubainika kukiuka Katiba ya chama hicho kwa kufungua kesi katika mahakama za kiraia.






