Monday , 29th Oct , 2018

Klabu ya soka ya Yanga inaendelea kukosa huduma ya nyota wake kadhaa ambao ni majeruhi, kuelekea mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara kesho dhidi ya Lipuli FC.

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera akiwa kwenye mazoezi na wachezaji wa timu hiyo. Kulia ni Ibrahim Ajibu.

Yanga ambayo ipo katika nafasi ya tatu, imethibitisha kuwakosa nyota wake ambao bado ni majeruhi, akiwemo Ibrahim Ajibu na Pappy Tshishimbi.

''Kuelekea mchezo wetu na Lipuli FC kesho, bado tunaendelea kuwakosa wachezaji wetu, Juma Mahadhi, Ibrahim Ajibu, Pappy Tshishimbi na Baruani Akilimali ambao wote bado wanasumbuliwa na majeraha'', imeeleza taarifa ya Yanga.

Yanga ambayo ilitoa mapumziko ya siku mbili baada ya mechi ya Alhamisi dhidi ya KMC, iliingia kambini jana Jumapili kujiwinda na mchezo wake dhidi ya Lipuli Fc utakaopigwa kwenye  uwanja wa Taifa kuanzia saa 1:00 usiku.

Yanga ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa na alama 22 baada ya mechi 8. Msimamo wa ligi kuu unaongozwa na Azam FC yenye alama 27 kwenye mechi 11, huku Simba wakiwa katika nafasi ya pili wakiwa na alama 23 kwenye mechi 10.