Friday , 17th Jun , 2016

Kikosi cha Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara timu ya Yanga kimeondoka nchini Uturuki kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo wao wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Mo Bejaia Juni 19.

Yanga waliweka kambi ya muda mfupi nchini Uturuki kwa ajili ya kuwavutia kasi Waalgeria katika mchezo wa ugenini ambao wanatakiwa kufanya vizuri ili kujiwekea mazingira mazuri katika mechi zake zinazofuata.

Meneja wa Yanga Hafidh Saleh amesema, maandalizi ya mchezo yamekamilika kwa asilimia kubwa na wamefanya mazoezi ya asubuhi, mchana na usiku kwa kuangalia ratiba ya mchezo ambao utachezwa usiku nchini Algeria.

Hafidh amesema, hakuna mchezaji ambaye amepata majeruhi kitu ambacho kinampa kocha kuwa na wigo mpana wa kuchagua nani wa kucheza katika mtanange huo.

Yanga ilikuwa kambini Uturuki kwa siku tano kujiandaa na mechi hiyo ya kwanza ya Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali itakayopigwa Jumapili.

Baada ya mchezo huo Yanga itarejea nyumbani kujiandaa na mchezo dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Juni 28 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.