Mabao mawili ya Yanga yamefungwa na Donaldo Ngoma aliyepewa pasi na Mzimbabwe mwenzake Thabani Kamusoko katika dakika za 31 na 34 na kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Mafunzo walijitutumua na kupeleka mashambulizi kadhaa likiwemo lililozaa penalti baada ya Kelvin Yondani kuachwa na kumvuta mshambuliaji wa Mafunzo, lakini kipa Deo Munishi ‘Dida’ akaipangua na baadaye kuidaka.
Paul Nonga aliyeingia dakika 10 za mwisho kuchukua nafasi ya Tambwe alifunga bao la tatu katika dakika ya 89 huku walinzi wa Mafunzo wakiamini alikuwa ameotea.
Mchezo wa pili uliwakutanisha Mtibwa Sugar na Azam Fc ambapo Mtibwa Sugar ndiyo alitawala sehemu ya mchezo kwa kiasi kikubwa huku ikipoteza nafasi nyingi za kufunga na kupelekea timu hizo kwenda mapumziko bila ya bao.
Azam FC ilionekana kuamka katika kipindi cha pili, lakini dakika tano tu za mwanzo na baada ya hapo, Mtibwa Sugar wakashika usukani tena hadi walipopata bao kupitia kwa Hussein Javu baada ya beki Said Morad kufanya makosa na mpira kumfikia Ramadhani Kichuya aliyempa mpira mfungaji.
Mtibwa Sugar wangeweza kupata mabao zaidi, lakini wakapoteza nafasi zaidi hadi Azam FC waliposawazisha bao kupitia kwa nahodha wake, John Bocco.
Bocco alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti, dakika chache tu baada ya kuingia na kuangushwa wakati akiwachambua mabeki wa Mtibwa Sugar.
Kichuya aliifungia Mtibwa Sugar bao safi katika dakika ya 88 akiunganisha krosi safi ya Baba Ubaya, lakini wakati mwamuzi akijiandaa kuweka mpira kati, mwamuzi msaidizi ambaye ni mwanamama, akasema mfungaji aliotea jambo ambalo lilizua taharuki.
Michuano hiyo itaendelea tena hapo kesho Uwanja wa Amaan kwa kupigwa mechi za kundi A ambapo katika mchezo wa awali timu ya JKU ya Zanzibar itavaana na URA ya Uganda saa kumi na robo jioni huku Simba SC wakivaana na Jamhuri ya visiwani humo majira ya saa mbili na robo usiku.
