
Katika mchezo wa leo ambao kwa kiasi kikubwa umetawaliwa na Yanga licha ya Stand kufuruka mara chache, Yanga imejipatia mabao yake kupitia kwa Donald Ngoma aliyefunga kwa kichwa akimalizia kros ya Saimon Msuva dakika ya 18, Saimon Msuva aliyefunga bao zuri katika 'impossible angle' upande wa kulia baada ya kupokea pasi kutoka kwa Ngoma dakika ya 26 na kuandika bao la pili.
Mengine yamefungwa na Obrey Chirwa dakika ya 46 na nahodha Nadir Haroub Canavaro, aliyefunga kwa kichwa kona iliyochongwa na Saimon Msuva.
Katika mchezo huo pia, Yanga imejikosesha ushindi mkubwa zaidi baada ya Saimon Msuva kupaisha mkwaju wa penati dakika ya 59, iliyopatikana baada ya yeye mwenyewe Msuva kuangushwa katika eneo la 18.
Saimon Msuva amefikisha jumla ya mabao 10 na sasa yeye ndiye kinara wa ufungaji msimu huu akiwapiku Shiza Kichuya na Amiss Tambwe (ambaye leo hajacheza) wakiwa na mabao 9 kila mmoja, huku Chirwa na Ngoma wakifikisha mabao 8 sawa na John Bocco wa Azam.
Ushindi huu unaifanya Yanga ifikishe point 49 na kuongeza wigo wa tofauti ya point kati yake na Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi zake 45.
Simba inashuka dimbani kesho mjini Songea kukabiliana na Majimaji, na endapo itashinda itapunguza 'gap' la point kuwa moja, lakini endapo haitapa ushindi, basi itakuwa ni sawa na kuibariki Yanga kuufukuzia ubingwa wa ligi kuu peke yake kulingana na kasi iliyonayo hivi sasa.