Sunday , 16th Sep , 2018

Klabu ya soka ya Yanga, leo inashuka dimbani leo kukipiga na Stand United ya Shinyanga, kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara, ambapo Yanga inabebwa na rekodi yake nzuri dhidi ya timu hiyo maarufu Chama la wana.

Mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo.

Rekodi ya timu hizo mbili inaonesha tangu timu ya Stand United ipande ligi kuu msimu wa 2014/15, zimecheza mechi 8 ambapo Stand United imeshinda mechi 1 pekee huku Yanga ikishinda mechi 7.

Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza tarehe 25/10/2014 ambapo Yanga ilishinda mabao 3-0. Kisha zikakutana tarahe 21/04/15 na Yanga ikashinda 3-2.

Msimu wa 2015/16 zilikutana tarehe 09/12/2015 ambapo Yanga ilishinda mabao 4-0 kabla ua kushinda tena mabao 3-1 kwenye mechi iliyopigwa tarehe 03/05/2016.

Katika msimu wa 2016/17 Stand United ilipata ushindi kwa mara ya kwanza dhidi ya Yanga ikifunga bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Kambarage Shinyanga. Timu hizo tena zikakutana msimu huo ambapo Yanga ilishinda mabao 4-0.

Msimu uliopita wa 2017/18 Yanga ilianza kwa kushinda mabao 4-0 kabla ya mechi ya pili kushinda 3-1. Mchezo wa leo utapigwa saa 10:00 jioni. Yanga imeshacheza mechi moja na kushinda huku Stand United nayo ikicheza mechi mbili na kushinda zote.