Msemaji wa Azam FC Jaffery Iddy Maganga amesema, kinda huyo mwenye miaka 18 ametua baada ya kulivutia Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, ambaye amependekeza asajiliwe baada ya kumuona Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Medeama ikiilazimisha sare ya bao 1-1 Yanga katika mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Maganga amesema, wamefanya jitihada za hali ya juu hadi kunasa saini yake, ambapo alilazimika kumfuata mshambuliaji huyo hadi mjini Takoradi, Ghana, ambapo usajili huo umeratibiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, aliyemfuata kukamilisha kazi hiyo maalum kwa kuzungumza na pande zote mbili mchezaji na uongozi wa Medeama akiwemo Mmiliki wa timu.
Maganga amesema, akiwa nchini Ghana, Kawemba alipata fursa ya kukutana na kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ghana ‘Black Stars’, Avram Grant raia wa Israel, wakati wa mchezo wa marudiano kati ya Medeama na Yanga ulioisha kwa wenyeji kushinda mabao 3-1.
Maganga amesema, katika mazungumzo yake na Kawemba, Grant aliyewahi kuifundisha Chelsea na kuifikisha kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008, aliipongeza Azam FC kwa kutambua kipaji cha Enock na kumsajili.
Azam FC hivi sasa ipo kwenye kambi visiwani Zanzibar ikifanya maandalizi kabambe ya kujiandaa na msimu ujao, kikosi kikiwa chini ya makocha wapya kutoka nchini Hispania.



