Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Klabu ya Yanga akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani.
Uchaguzi Mkuu wa Yanga ulipangwa awali kufanyika Mei 27, mwaka huu lakini ukasogezwa mbele mpaka kati kati ya Juni na Kamati ya TFF ambapo mchakato wake umeanza rasmi juzi ikiwa ndio siku ya kuanza kutoa fomu kuashiria kuanza kwa mchakato huo rasmi.
Ikumbukwe Baraza la Michezo nchini BMT lilitoa siku 90 kwa klabu hiyo kuhakikisha mpaka Juni 30 mwaka huu inakuwa imepata viongozi wake halali wakuchaguliwa na wanachama halali katika mkutano halali kwa mujibu wa Katiba itakayotumika chini ya usimamizi wa karibu wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF.
Uamuzi huo wa Baraza la Michezo kuipa TFF usimamizi wa moja kwa moja wa uchaguzi huo umetokana na klabu ya Yanga kutokuwa na viongozi halali kwa mujibu wa Katiba kwani waliopo sasa hawatambuliki kikatiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali amesema kama kuna baadhi watapiga kura na wengine kuachwa, haitakuwa sawa sawa.
"Kama wengine watapiga wakiwa na kadi za zamani na kuwaacha wale wenye kadi za uanachama za Benki ya Posta, haitakuwa sawa kabisa," alisema Mzee Akilimali na kuongeza, "Wapo waliokuwa wana kadi za zamani, wakabadili na kuchukua zile za Benki ya Posta. Wengine kweli ni wapya, sasa kuwaacha wengine na wengine wapige ni kuleta mgogoro,".
Pia Baraza hilo limeomba BMT na TFF kuitishwa mkutano wa dharura wa klabu hiyo ambao utahusiana na masuala ya uchaguzi.
"Pia ninaomba kama watakubali katika mkutano huo pia wawashirikishe watu kutoka wizara ya michezo, viongozi wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA)," aliomba Mzee Akilimali.