Friday , 2nd Dec , 2016

Baraza la wazee wa Klabu ya Simba wamezuia mkutano wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Desemba 11 mwaka huu jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Klabu ya Simba, Hamis Kilomoni

 

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Klabu ya Simba, Hamis Kilomoni amesema, wamepokea barua za malalamiko kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo wakidai kutokushirikishwa katika mambo mbalimbali yanayotendeka ndani ya klabu hiyo hususani mkutano huo.

Ameongeza kuwa hata wao wamekuwa hawashirikishwi hivyo wameamua kuzuia mutano huo kwani una kila dalili za uvunjifu wa amani kutokana na mgawanyiko wa wanachama pamoja na chuki zilizopandikizwa kama ilivyokuwa katika mkutano wa awali ambapo Rais wa Klabu hiyo Evance Aveva alitolewa kwa ulinzi mkali.

Kilomoni amesema, lengo la kuzuia mkutano huo ni kutaka uhakiki wa wanachama wote ufanyike kupitia msajili wa vyama vya michezo na vilabu kwa sababu katika mkutano wa Julai 31 mwaka huu watu wengi waliingia kwa risiti badala za kadi za uanachama.

Kilomoni ameomba Serikali iingilie kati mgogoro huo kwa ajili ya usalama wa nchi.