Wednesday , 11th Nov , 2015

Watanzania wametakiwa kujitokeza siku ya Jumamosi uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwapa hamasa wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars katika mechi dhidi ya Algeria.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Said Meck Sadiki amesema japo Algeria ni timu inayofanya vizuri Afrika lakini kwa juhudi katika mchezo huo hakuna litakaloshindikana.

Kwa upande wao wachezaji wa Klabu ya TP Mazembe ambao pia ni wachezaji wa Taifa Stars Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta wamewashukuru watanzania kwa sapoti yao walipokuwa katika Klabu lakini wamewataka nguvu zao katika kutoa sapoti wazielekeze Jumamosi katika mchezo wao dhidi ya Algeria.

Kwa upande wake Samatta amesema, Ubingwa alioupata wa ufungaji bora katika michuano hiyo umekwisha na kilichobakia ni jukumu lililo mbele yao la kupambana dhidi ya Algeria hivyo nguvu na uwezo alionao upo katika mechi dhidi ya Algeria kwa sasa.

Kwa upande wake Ulimwengu amesema, kombe la Klabu Bingwa Afrika wameliweka pembeni na hivi sasa wapo kwa ajili ya kupambana katika mechi dhidi ya Algeria ili kuweza kusonga mbele katika michuano hiyo ya kuwania kufuzu kwa fainali za kombe la dunia zitakazofanyika mwaka 2018 nchini Urusi.