Tuesday , 24th Nov , 2015

Shirikisho la soka nchini TFF limesema wasimamizi wa soka hapa nchini wanatakiwa kuhakikisha kila klabu ina leseni ili kuweza kushiriki mashindano ya Kimataifa yanayosimamiwa na shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa kozi ya siku mbili ya mafunzo ya leseni za vilabu inayoendeshwa na CAF, Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Cellestine amesema, uendeshaji wa mpira wa miguu duniani umebadilika katika nyanja zote za uongozi, miundombinu, suala linalochangia wao kama wasimamizi wa soka waweze kusimamia na kuhakikisha klabu zao zina elimishwa juu ya hilo.

Mwesigwa amesema, CAF katika kozi hiyo imetoa agizo kuwa vilabu vyote shiriki vya ligi kuu, daraja la kwanza na la pili vinavyoshiriki michuano ya kimataifa lazima viwe vimepata leseni hiyo ambayo itaipa nafasi ya kushiriki michuano inayoandaliwa na shirikisho hilo na kwa klabu ambayo haitatimiza mahitaji ya kupata leseni hiyo haitaweza kushiriki.

Mwesigwa amesema, Ili kupata leseni ya klabu, klabu inapaswa kutimiza vigezo vilivyowekwa ikiwemo masuala ya utawala, ripoti ya mapato na matumizi iliyokaguliwa, uwanja wa mazoezi.

Mwesigwa amesema, mmiliki mmoja wa klabu hatarusiwa kumiliki timu zaidi ya moja kwenye ligi moja, kila klabu lazima iwe na program za vijana na uwanja wa mazoezi.