Saturday , 28th Jun , 2014

Hatimaye baada ya mvutano wa takribani majuma matatu katika mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa viongozi wa klabu ya soka ya Simba, kesho uchaguzi huo uliokuwa na vibweka vingi katika mchakato wake utafanyika jijini Dar es salaam

Baadhi ya wanachama wa kabu ya Simba wakiwa jukwaani kushuhudia moja ya michezo ya timu hiyo.

Hii leo kampeni za kunadi sera zao kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa viongozi wa klabu ya Simba uchaguzi ambao utafanyika kesho kuanzia saa 3 asubuhi katika ukumbi wa bwalo la maofisa Polisi Oysterbay jijini Dar es salaam zimehitimishwa hii leo

Katika kuhitimisha kampeni hizo hii leo kundi la marafiki wa klabu ya Simba wamejitokeza katika ufungaji wa kampeni kwa kumuunga mkono mgombea urais wa klabu hiyo Evans Aveva

Ambapo mwenyekiti wa kundi hilo maarufu kama Friends of Simba Zakaria Hans Pope amesema wameamua kurejea kundini kutokana na nafasi ya urais kuwaniwa na mtu sahihi ambaye wao wanamuunga mkono na kuchaguliwa kwa mgombea huyo wanaamini kutaleta umoja na kuunda Simba mpya na hatimaye kuwarejesha kundini wale wote ambao waliamua kujiweka pembeni na klabu hiyo kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri na uongozi ambao kesho unaondoka rasmi madarakani

Na kwa upande wake Evans Aveva ambaye anagombea nafasi ya urais wa klabu ya Simba pamoja na sera zote alizonadi kwa wanachama katika matawi mbalimbali aliyopita kujinadi amesema yuko tayari kuungana na kufanya kazi na kiongozi yeyote atakayechaguliwa na wanachama wa klabu hiyo hapo kesho ndio maana ameamua kuwaalika wagombea wote katika kutamatisha kampeni zake.