Sunday , 29th Jan , 2017

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na idara ya michezo ya Wazara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) limeanzisha kampeni maalum ya kuelekea katika michuano ya Olimpiki mwaka 2020, Japan

Jamal Malinzi, Rais wa TFF

Kampeni hiyo inazinduliwa kesho Jumatatu Januari 30, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari; Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Makamu Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau

Uzinduzi wa kampeni hizo unaopewa jina la ‘The Road to Tokyo 2020’ utafanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na kushirikisha wadau na wafamilia wa mpira wa miguu Tanzania.

Tayari timu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 23 ‘Kilimanjaro Warriors’ imeingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya awali ya kucheza mechi za kufuzu fainali hizo za za Olimipiki.

Kambi hiyo imepigwa kwenye Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambako pia kuna Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazoezi kulingana na program za walimu.

Tanzania haijapata kushiriki Michuano ya Olimpiki kwa upande wa mpira wa miguu jambo ambalo limeisukuma TFF kuona kuwa ni fursa ya mpira wa miguu kuchezwa hivyo inashirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kufanikisha mipango na taratibu.