Friday , 20th Feb , 2015

Timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni (Beach Soccer) kesho itacheza mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya Taifa ya Kenya, mchezo utakaoanza majira ya saa 10 jioni kwenye fukwe za Escape One Club Msasani jijini Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini, Baraka Kizuguto amesema timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni kutoka nchini Kenya wanatarajia kuwasili leo jioni jijini Dar es salaam, tayari kabisa kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano.

Kizuguto amesema, waamuzi wa mchezo huo watakuwa ni Beye Mbokh kutoka Senegal, mwamuzi wa pili ni Signate Youssouph pia kutoka nchini Senegal, mwamuzi wa tatu ni Maolidy Tsaralaza kutoka Madagascar, mtunza muda atakuwa Hachim Said Nassur kutoka nchini Madagascar na kamishina wa mchezo atakuwa Roch Henriette kutoka Visiwa vya Shelisheli.

Kizuguto amesema, Tayari waamuzi wa mchezo huo wameshawasili jijini Dar e salaam tangu jana jioni tayari kwa mchezo huo, na endapo timu ya Taifa ya Tanzania itasonga mbele, itakutana na timu ya Taifa ya Misri kati ya Machi 7, 8 na kurudiana kati ya Machi 13, 14, 2015.

Fainali za Soka la Ufukweni zinatarajiwa kufanyika mapema mwaka huu katika Visiwa vya Shelisheli.