
Matokeo hayo, yanaifanya Taifa Stars itolewe kwa jumla ya mabao 9-2, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 na Mbweha hao wa Jangwani katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jumamosi mjini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Algeria walipata bao lao la kwanza mapema tu sekunde ya 43 dakika ya kwanza, mfungaji Yacine Brahimi, aliyemalizia krosi ya Mesloub Walid aliyempita beki wa kushoto Mwinyi Hajji Mngwali, baada ya Himid Mao kupokonywa mpira.
Algeria walipata bao la pili dakika ya 23 kupitia kwa Ghoulam Faouzi aliyepiga shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa zaidi ya mita 20, baada ya kiungo Mudathir Yahya kumchezea rafu Mesloub Walid na kuoneshwa kadi ya njano.
Mshambuliaji Elias Maguri aliifungia Taifa Stars bao dakika ya 27 kwa shuti la mbali nje ya 18, lakini pamoja na refa Alioum Alioum kuelekea kukubali, akaghairi baada ya ushauri wa msaidizi wake namba mbili, Noupue Nguegoue.
Mudathir Yahya alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 40 baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 40 kwa kumkwatua Yacine Brahimi.
Na Mahrez Ryad akaifungia Algeria bao la tatu dakika ya 41 kwa shuti kali, akimalizia krosi ya Islam Slimani.
Kipindi cha pili, kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na mabadiliko akiwatoa kipa Ally Mustafa Barthez na winga Farid Mussa na kuwiangiza kipa Aishi Manula na kiungo Salum Telela.
Mabadiliko hayo hayakuwa na msaada wowote kwa Taifa Stars, kwani Algeria ilinufaika zaidi kipindi cha pili kwa kupata mabao manne zaidi.
Islam Slimani alifunga bao la nne dakika ya 48 kwa penalti baada ya Mahrez kugongana na beki wa Taifa Stars, Kevin Yondan.
Ghezzal Faouzi akafunga bao la tano dakika ya 58 kwa penalti baada ya Slimani kugongana na Aishi Manula kwenye boksi wakigombea mpira.
Nahodha wa Mbweha wa Jangwani, Carl Medjani akafunga bao la sita kwa kichwa akimalizia kona ya Mahrez.
Ghezzal Rachid aliyetokea benchi akafunga bao la saba dakika ya 74 akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu wa Mahrez.
Taifa Stars ikazinduka baada ya bao hilo na kukaribia kufunga mara mbili, kupitia kwa washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Dakika ya 85 Ulimwengu alimpa pasi nzuri Samatta baada ya wawili hao kugongeana vizuri, lakini Mbwana akapiga nje.
Na dakika ya 89, Maguri alimpa pasi nzuri Ulimwengu akafanikiwa kumtoka beki Carl Medjani, lakini kipa M’bolhi Rais akaugusa mpira kidogo na kutoka nje, ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.