
Mshambuliaji, Adi Yussuf (kinyozi) akiwanyoa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kuelekea mchezo dhidi ya Senegal
Mchezo huo utakuwa ni wa kwanza kwa Taifa Stars katika hatua ya makundi ya michuano hiyo tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980 nchini Nigeria.
Kuelekea mchezo huo, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema kuwa wanafahamu ubora wa Senegal lakini na wao hawatokwenda uwanjani kuwatazama tuu bali watahakikisha wanapambana nao ili mwenye kiwango bora ashinde mchezo.
"Ukizungumzia mpira wa Afrika huwezi kuacha kuitaja Senegal lakini haina maana tutaenda uwanjani kuwaangalia wafanye wanachotaka. Kabla ya filimbi ya mwisho nadhani kila timu inanafasi", amesema Mbwana Samatta.
Naye kocha mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amesema kuwa timu yake imejiandaa vya kutosha kuelekea mchezo huo huku ikiwaheshimu Senegal kutokana na kiwango walichonacho kuzidi wao.
Mchezo huo utapigwa majira ya saa 2:00 usiku. Timu mbili za Afrika Mashariki, Uganda na Burundi zimecheza michezo yao ya kwanza hapo jana, ambapo Uganda imefanikiwa kuichapa Congo DR kwa mabao 2-0 na kuongoza kundi A, huku Burundi ikipoteza 1-0 mbele ya Nigeria.