Wednesday , 8th Jun , 2016

Klabu ya Stand United ya Mjini Shinyanga imesema, inahakikisha inakaa kwa ajili ya kuangalia ni kitu gani wanatakiwa kufanya katika kuboresha kikosi kwa ajili ya kupambana na ushindani wa Ligi kuu msimu ujao.

Kikosi cha Stand United

Mkurugenzi wa ufundi wa Stand United Muhibu Kanu amesema, wamejaribu kuangalia ripoti ya kocha Patrick Liewing na wamegundua maeneo ambayo yanatakiwa kuyafanyiwa marekebisho ikiwa ni katika upande wa magoli kipa,eneo la ulinzi, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji pamoja na kumuongezea nguvu mshambuliaji Elias Maguli.

Kanu amesema, wameanza kuangalia wachezaji walio ndani ya vilabu vya Simba na Yanga ambao wanaamini ni wazuri na wameshamaliza mikataba yao ndani ya Klabu hizo.

Kanu amesema, pia wameangalia wachezaji wa nje ya nchi kama Cameroon na Ivory Coast ambapo wapo mawakala ambao wameshapewa kazi ya kuhakikisha wanaangalia na kupata wachezaji watakaoweza kukiboresha kikosi cha Stand United kwa msimu ujao.

Kanu amesema, wanaamini kwa usajili watakaoufanya utawawezesha kushika nafasi mbili za juu katika msimu ujao wa Ligi Liu ya Soka Tanzania Bara.
Kanu amesema, yote yanawezekana kwani wanakikosi kipana na wanabajeti yakutosha ya kuweza kufanya vurugu kubwa kwenye usajili kwa kumsajili mchezaji wanaomuhitaji.