
Wadau wengi wa soka waliitabiria klabu hiyo kufanya vizuri kwa miaka kadhaa mbeleni, wengine wakiitaja kuja kuwa klabu ya nne kwa ubora itakayosimama pamoja na Simba, Yanga na Azam Fc kutokana na mipango mizuri ya viongozi wake pamoja na usajili wa wachezaji wenye ubora wa hali ya juu ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo walioisaidia kufikia mafanikio hayo msimu uliopita.
Mambo yakaanza kuwa tofauti mapema kabla ya msimu huu kuanza ambapo wachezaji wake muhimu wengi waliondoka klabuni hapo huku Singida United ikiwasajili wachezaji wa kiwango cha chini tofauti na ambao iliwauza. Hali hiyo imeendelea hata baada ya msimu wa ligi kuanza, ikishuhudiwa klabu hiyo ikipata matokeo yasiyoridhisha ambapo mpaka sasa imeshacheza michezo sita na kuambulia alama saba pekee.
Hali ya kiuchumi pia imeshuka kwa klabu hiyo msimu huu hali inayopelekea wachezaji wake wengi na baadhi ya makocha kugomea kuendelea kuitumikia klabu hiyo wakidai stahiki zao. Mlinda mlango wake, Peter Manyika Jr alijiengua katika klabu hiyo kutokana na kutolipwa fedha zake za usajili na mishahara kwa miezi kadhaa.
Hivi karibuni pia kumekuwa na tetesi za makocha wawili wasaidizi wa klabu hiyo, Jumanne Challe na Athuman Mfaume kujiengua klabuni hapo kutokana na kutolipwa stahiki zao pamoja na kutopewa mikataba licha ya kuhudumu kwa muda mrefu, huku tetesi zingine zikieleza kuwa wadhamini wa klabu nao wako katika harakati za kujiondoa.
Mpaka sasa imeshapoteza ule umaarufu wa msimu uliopita na mategemeo yale yaliyokuwa yakifikiriwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka yanazidi kupungua siku hadi siku kutokana na timu hiyo kutokuwa na ushindani kuanzia ndani ya hadi nje ya uwanja huku mwisho wa changamoto hizo ukiwa haujulikani.