Kikosi cha wachezaji wa Simba wakiomba dua katika moja ya michezo ya timu hiyo msimu uliopita.
Uongozi wa klabu ya Simba umesema bado haujafunga zoezi la usajili kwa wachezaji wa ndani na nje nchi, makamu wa Rais wa klabu hiyo Geoffrey Nyange Kaburu amesema kumekuwa na taarifa nyingi juu ya usajili wa baadhi ya wachezaji hasa wa kigeni kwamba tayari timu hiyo imeshakamilisha zoezi hilo kitu ambacho si sahihi
Kaburu amesema mpaka sasa wamesajili wachezaji wa kigeni wanne kati ya watano na hivyo wamebakisha nafasi moja ambayo pengine ikajazwa na mmoja kati ya wachezaji watatu wa kigeni ambao watawasili nchini kuanzia jioni ya leo
Wachezaji ambao mpaka sasa wameshamwaga wino mpaka sasa ni mganda Joseph Owino, warundi Amis Tambwe na Piere Kwizera na mkenya Donald Musoti
Aidha Kaburu amesema wachezaji hao watatu ambao watafanya majaribio ya kusaka nafasi moja wanatoka katika nchi za Kenya, Botswana na Gabon huku pia akithibitisha kumnyakua beki tegemeo wa wagosi wa kaya Coastal Union ya Tanga Abdul Banda
Kwa upande mwingine uongozi wa Simba umesema umekuwa ukipokea na kuwaondoa katika majaribio baadhi ya wachezaji wa ndani na wa nje wanaofika katika mazoezi ya timu hiyo kufanya majaribio kutokana na sababu za kiafya.
Makamu wa Rais wa klabu ya hiyo Geoffery Nyange Kaburu amesema pamoja na baadhi yao kuonesha uwezo mkubwa katika majaribio lakini suala la afya huwa linapewa kipaumbele na hii ni utaratibu wa soka duniani kote ukitambuliwa na FIFA, CAF na TFF na hivyo hata wao watasajili mchezaji ambaye yuko fiti kiafya