Nape Nnauye akiongea na vyombo vya habari katika uwanja wa Taifa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, ndiye aliyetoa tamko hilo leo wakati akifanya ziara uwanjani hapo kukagua uharibifu huo na kukemea tabia hiyo ya mashabiki.
Amesema timu zote mbili zinahusika kwa kuwa mashabiki wamevunja mageti ya pande zote mbili, yaani upande wa Simba na upande wa Yanga, mageti ambayo yalivunjwa wakati mashabiki hao wakilazimisha kuingia ndani ya uwanja baada ya mfumo wa tiketi wa kielektroniki kushindwa kufanya kazi.
Uharibifu mwingine alioushudia ni ule wa viti kung’olewam ambapo mashabiki wa Simba ndiyo wanaotajwa kuhusika na ung’oaji wa viti hivyo mara baada ya Yanga kupata bao lililofungwa na Amis Tambwe, wakidai kuwa halikuwa bao halali.
Waziri Nape amesema mara baada ya mchezo yeye na timu yake walibaki uwanjani hadi usiku na kuhesabu viti vilivyoharibiwa, ambapo walibaini kuwa zaidi ya viti 1,700 vilikuwa vimeng’olewa.
Kufuatia uharibifu huo, Nape amesema mgao wa mapato yaliyotokana na mechi hiyo kwa vilabu hivyo yatazuiwa kwa muda hadi tathmini itakapofanyika ili kubaini gharama ya matengenezo ya uwanja huo.
Kufuatia uharibifu huo, Nape amesema kuwa Rais Magufuli ambaye alikuwa akiufuatilia mchezo huo, ameeleza kukasirishwa sana kitendo cha mashabiki kuharibu uwanja huo na kuagiza wahusika wachukuliwe hatua.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo mwenye dhamana na michezo nchini amesema kuwa serikali ina mpango wa kufunga kamera maalum uwanjani hapo ili kuwabaini mashabiki wenye wanaofanya uharibifu ili wawajibike wao moja kwa moja badala ya kubebesha mzigo vilabu vyao.