Sunday , 11th Feb , 2018

Klabu ya soka ya Simba imefanikiwa kuibuka na suhdini wa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Gendarmerie Tnale ya Djibouti kwenye mchezo wa kombe la shirikisho barani Africa.

Mchezo huo ambao umemalizika jioni hii kwenye uwanja wa taifa mabao ya Simba yamefungwa na kiungo Said Ndemla dakika ya kwanza na John Bocco mawili dakika za 32 na 45 na Emmanuel Okwi dakika ya 90.

Simba leo ilikuwa inarejea kwenye michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2012/13 ambapo iliondolewa na timu ya Recreativo de Libolo ya Angola.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa huko Djibouti kati ya Februari 20 na 21, 2018 ambapo waamuzi kutoka Burundi na Kamishna wa mchezo atatokea nchini Rwanda.

Hapa nyumbani Simba inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na alama 41 baada ya mechi 17 mbele ya watani wao wa jadi Yanga wenye alama 34 katika nafasi ya pili.