Mfungaji wa bao la pili la Serengeti Boys, Ibrahim Abdallah akishangilia goli hilo.
Timu ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ambayo wiki chache zilizopita ilionesha maajabu katika michuano ya mabara iliyofanyika nchini India na kushika nafasi ya tatu huku ikimaliza michuano hiyo bila kupoteza mchezo zaidi ya kushinda na kutoka sare hii leo kwa mara nyingine imeonesha ubora wake baada ya kuitambia timu ya Shelisheli katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Serengeti Boys ambayo inaundwa na vijana ambao hawachezi ligi yoyote wakitokea katika vituo vya kukuza michezo na wengi wao wakiibukia katika mashindano ya Airtel Rising Stars na Copa Coca cola imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Shelisheli katika mchezo wa kwanza wa raundi ya Kwanza kufuzu Fainali za vijana chini ya miaka 17 [U17] barani Afrika mwakani zitakazopigwa nchini Madagascar.
Baada ya ushindi huo, Serengeti Boys sasa itahitaji kwenda kulazimisha matokeo ya sare ya aina yoyote ama isifungwe goli zaidi ya 2-0 kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo nchini Shelisheli ili kukata tiketi ya kwenda kukutana na Afrika Kusini katika mchezo wa mwisho utakaoamua hatima ya timu hiyo kuelekea katika fainali hizo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Belay Tadesse Asserese, aliyesaidiwa na washika vibendera Tigle Giza Belachew na Kinfe Yilma Kinfe wote wa Ethiopia, ambapo hadi mapumziko, Tanzania [Serengeti Boys] walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Nickson Kibabage alianza kuifungia timu ya kocha Bakari Nyundo Shime dakika ya 15 kwa shuti la umbali wa mita 19 kutoka upande wa kushoto wa Uwanja baada ya kupokea pasi ya Zubeiry Ada.
Shelisheli wakarudi nyuma ‘kupaki basi’ baada ya baada ya bao hilo ili kujizuia kuruhusu mabao zaidi ya ugenini na kuwapa wakati mgumu kidogo wenyeji.
Hata hivyo, Ibrahim Abdallah Ali alifanikiwa kuifungia bao la pili dakika ya 22 Serengeti Boys inayonolewa pia na Mshauri wa Ufundi wa Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF) kwa program za Vijana, Mdenmark Kim Poulsen.
Ibra Ali alifunga bao hilo baada ya kuupitia mpira uliomponyoka kipa wa Shelisheli, Juninho Mathiot kufuatia shuti dhaifu la Kibabage, aliyekuwa anapanda mno kusaidia mashambulizi licha ya kucheza beki ya kushoto.
Serengeti Boys ilipoteza nafasi mbili zaidi za kufunga baada ya kuwa inaongoza kwa mabao 2-0 kabla ya mchezo kwenda mapumziko
Katika kipindi cha pili, Serengeti Boys walifanikiwa kuunenepesha ushindi wao kwa bao la tatu lililofungwa kwa penalti na beki wa kati Ally Hussein Msengi dakika ya 62, baada ya beki wa Shelisheli, Stan Esther kuunawa mpira wa adhabu wa Asad Ali Juma katika ukuta.
Serengeti Boys iliendelea kulisakama lango la wageni wao, lakini hawakufanikiwa kupata mabao zaidi na hasa dakika za lala salama baada ya kuonekana wakicheza taratibu tofauti na kasi ile waliyoingia nayo kipindi cha kwanza na sasa wakawa wakionekana kama wameridhika na wameshamaliza kazi jambo ambalo makocha wa timu hiyo wanatakiwa walifanyie kazi.