Thursday , 20th Sep , 2018

Mshambuliaji wa klabu ya KRC Genk na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anatarajia kutupa karata yake ya kwanza katika mchezo wa hatua ya makundi ya michuano ya ‘Europa League’ hii leo.

Mshambuliaji, Mbwana Samatta na kiungo, Leandro Trossard.

Genk itakuwa nyumbani ikiikaribisha Malmo ya nchini Sweden, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2016/17 ambapo iliishia katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Samatta amekuwa na msimu mzuri mpaka sasa katika michuano mbalimbali kwenye klabu yake, ikiwemo ya kufunga mabao tisa katika michezo sita mfululizo na anategemea kuwa mshambuliaji tegemeo katika kikosi kitakachoanza kwenye  mchezo huo.

Rekodi kuelekea mchezo huo zinaonesha kuipa nafasi Genk ya kuibuka na ushindi kwasababu ya uzoefu wake ikilinganishwa na klabu hiyo ya Malmo, ambapo mchezo huo utakuwa ni wa kwanza wa kimashindano kuzikutanisha timu hizo na mara ya kwanza kwa Genk kucheza na timu za Sweden katika michuano ya Ulaya.

KRC Genk imeshinda michezo yote ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Europa League, ikishinda kwa uwiano wa mabao 22-6, timu nyingine iliyoshinda michezo yote ya hatua hiyo ni Sevilla ya Hispania.

Malmo ni klabu changa katika michuano hiyo, msimu huu ni wa pili kwa klabu hiyo kushiriki na mara ya kwanza tangu 2011/12, ikiwa imepoteza jumla ya michezo mitano kati ya sita kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo huku wakiambulia sare moja pekee.

Genk iko katika kundi L pamoja na, Besiktas ya Uturuki, Malmo FFF ya Sweden na Sarpsborg 08 ya nchini Norway.