Bondia Said Mbelwa.
Kufuatia kusababisha kuvunjika kwa pambano la kuwania ubingwa wa kimataifa wa uzito wa Super Midle unaotambuliwa na UBO alipocheza na Kalama Nyilawila Jumamosi ya tarehe 24 mwezi huu, bondia Said Mbelwa amefungiwa kwa miezi sita na vyama mbalimbali vya masumbwi ya kulipwa hapa nchini.
Katibu mkuu wa PST ambao ndio walikuwa wasimamizi wa pambano hilo, bwana Anthony Luta , amethibisha hilo akizungumza na EATV.
Bwana Luta amesema baada tu ya pambano lile, walipokea barua kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) likiwataka kuchukua hatua kwa waliohusika na vurugu hizo.
Luta ameongeza kwamba wakakutana na vyama vingine vya masumbwi ya kulipwa kama TPBC na TPBO na kukubaliana kwa kauli moja ya kumfungia Mbelwa kwa miezi sita kufanya shughuli za masumbwi hapa nchini.
Said Mbelwa alipata nafasi ya kuwania ubingwa huo baada ya kuumia kwa Thomas Mashali ambaye ndiye aliyeandaliwa kupambana na Kalama Nyilawila.
Oktoba 30, 2012, Said Mbelwa alipanda ulingoni nchini Afghanstan katika pambano maalumu la kuhamasisha amani nchini humo.
Licha ya kwamba alipoteza pambano hilo kwa KO dhidi ya Hamid Rahimi wa nchi hiyo, Mbelwa aliweka rekodi ya kupigana pambano la kwanza kabisa la masumbwi ya kulipwa katika historia ya nchi hiyo.