Thursday , 21st Jan , 2016

kocha mkuu wa timu ya ngumi ya Ngome ya jijini Dar esalam Hassan Mzonge amesema kwa sasa anawapa vijana wake mazoezi ya kutosha zikiwemo mbinu na ufundi ili waweze kuibuka washindi wa mashindano ya wazi ya Taifa yanayotarajiwa kuanza februari sita.

kocha mkuu wa timu ya ngumi ya Ngome akitoa mafunzo kwa mmoja ya mabondia watakaopanda ulingoni februari sita mwaka huu kwenye mashindano ya wazi ya Taifa

Akizungumza na East Africa Radio Mzonge amesema vijana wake 11 wapo katika maandalizi ya mwisho kabla ya kupanda ulingoni kwenye mashindano hayo ya Taifa yatakayofanyika Kawe jijini Dar es salaam.

Mzonge amesema licha ya ubingwa wa mashindano hayo wao kama Ngome wamekusudia kuonyesha mchezo mzuri utakaotoa taswira kwa watanzania kuwa wanauwezo wa kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Olimpiki baadae mwaka huu nchini Brazil.

Katika hatua nyingine nahodha wa timu hiyo Selemani Kidunda amesema wapo imara na kwa sasa hakuna majeruhi kwenye kikosi chao hivyo wadau wajitokeze kwa wingi kushuhudia mashindano hayo yatakayojumuisha mabondia kutoka kila kona ya nchi.