Twiga Stars inakabiliwa na mashindano ya kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Zimbabwe tarehe Machi nne jijini Dar-es salam na ule wa marudiano tarehe Machi 19 au 20 mwaka huu Harare nchini Zimbabwe.
Nassra Juma amechukua mikoba hiyo kufuatia aliyekuwa kocha mkuu wa Twiga Stars Rogasian Kaijage kuamua kukaa pembeni.
Kabla ya Kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Nassra aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Twiga Stars tangu mwaka 2011 akimsaidia kocha Charles Boniface Mkwasa na kipindi cha mwisho akamsaidia Rogasian Kaijage.
Nassra pia ni mwalimu wa timu ya Taifa ya Zanzibar ya soka la Wanawake (Zanzibar Soccer Queens) wakati huo huo pia ni kocha wa Women Fighter ambayo inashiriki ligi kuu soka ya Zanzibar kwa soka la wanawake, pia ni mwalimu mkuu wa timu ya Uhamiaji ya wanaume inayoshiriki ligi daraja la 2 taifa Unguja.
Nassra Juma ni miongoni mwa makocha wawili Visiwani Zanzibar mwenye Leseni ya juu ya ukocha wa shirikisho la soka barani Afrika (CAF) ambapo ana leseni ‘A’ sambamba na Hemed Suleiman Morocco kocha msaidizi wa Taifa Stars.
Kwa Tanzania nzima Nassra ni mwanamke pekee mwenye leseni ya juu ya ukocha ambayo anayo ‘A’ ya CAF na ‘B’ ya UEFA.




