Thursday , 7th Mar , 2019

Mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania wameombwa kutokuwa na wasiwasi juu ya maandalizi ya kikosi cha Taifa Stars kwaajili ya mchezo wa mwisho wa kufuzu michuano ya AFCON.

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Ammy Ninje alipokuwa akizungumzia maandalizi ya ujumla ya kikosi cha Taifa Stars dhidi ya Uganda kuelekea mchezo huo wa mwisho, ikizingatiwa kuwa Uganda wameshaanza maandalizi kwa kutaja kikosi chake.

"Kila nchi ina utaratibu wake wa kufanya kazi, wao wameanza na sisi tulishaanza tangu zamani, ingawa wao wametangaza wazi kwenye media lakini na sisi tutatangaza labda wiki ijayo", amesema Ammy Ninje.

"Mwalimu ameshakaa na walimu wake wamejadili watu wao watakaowahitaji lakini mwalimu Amunike akiwa tayari atataja kikosi chake", ameongeza.

Aidha Mkurugenzi huyo wa TFF ameeleza mipango ya kuongeza wachezaji wengi wanaocheza nchi za kigeni ziko vizuri huku akisema suala la uraia pacha ndiyo changamoto inayowakabili wachezaji wengi.

Taifa Stars ipo kundi L pamoja na Cape Verde, Lesotho pamoja na Uganda, ambapo kundi hilo linaongozwa na Uganda ambayo tayari imeshafuzu michuano hiyo itakayopigwa mwakani nchini Misri, huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Lesotho yenye alama tano sawa na Taifa Stars iliyo katika nafasi ya tatu kwa alama 5.

Endapo Taifa Stars itaibuka na ushindi katika mchezo huo wa mwisho dhidi ya Uganda, itakuwa na jumla ya alama 8 huku ikiombea Lesotho kupoteza au kutoka sare na Cape Verde, basi itakuwa imeshajinyakulia tiketi ya kushiriki michunao hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za TFF, leo Ijumaa ya Machi 8, 2019 kocha mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike anatarajia kutangaza kikosi kamili kitakachojiwinda dhidi ya Unganda 'The Cranes' katika mchezo wa mwisho wa kufuzu AFCON.