Thursday , 10th Sep , 2015

Timu ya Mbeya City 'Wagonga Nyundo wa Mbeya' wamesema Kagera Sugar itaoga mvua ya magoli wakati wa mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu ya Soka Tanzania Bara Jumamosi ya wiki hii uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Msemaji wa Mbeya City Dismas Ten amesema timu yao ina kila sababu ya kuendeleza ubabe wake dhidi ya Kagera Sugar kwa kuwa tayari inafahamu mapungufu ya timu hiyo.

Katika mchezo huo, Mbeya City itashuka dimbani huku ikijivunia rekodi yake ya kutopoteza mchezo hata mmoja kwenye mapambano ya msimu uliopita baina ya timu hizo.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza katika msimu uliopita uliopigwa Uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba, Mbeya City ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar iliyokuwa nyumbani ambapo katika mchezo wa mzunguko wa pili uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mbeya City iliendeleza ubabe kwa kuilaza Kagera mabao 2-0.