Wednesday , 16th Sep , 2015

Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es salaam DAREVA kimesema, kimeanza kupata muelekezo mzuri katika kozi ya waamuzi wa mpira wa wavu wa Ufukweni baada ya kutoa elimu hiyo kwa vitendo.

Mwenyekiti wa kamati ya Ufundi DAREVA Nassoro Sharif amesema, wanaamini washiriki wa kozi hiyo wataleta mabadiliko makubwa katika mchezo huo hususani katika mashindano ya mkoa yanayotarajiwa kuanza Mwishoni mwa mwezi huu.

Sharif amesema, wamepata washiriki 15 tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wanatarajia kuwa na washiriki 30 lakini wanaamini hapo mwakani watakuwa na washiriki wengi zaidi katika kozi mbalimbali kwani watu wengi watakuwa wameshakuwa na uelewa juu ya mchezo huo.

Kwa upande wake mmoja wa wakufunzi wa mchezo huo khalid Rashid amesema, mpaka sasa mchezo huo unazidi kukua zaidi kutokana na mafunzo hayo japo kuna mapungufu machache ambayo ni ya kibinadamu ambayo yanaweza kurekebishika.

Khalid amesema, mchezo huo utaendelea kukua zaidi kwani katika mafunzo hayo wameweza kupokea washiriki ambao ndiyo mara yao ya kwanza kujifunza mchezo huo ambao wanaamini watakapomaliza mafunzo hayo watakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali.