Monday , 4th Feb , 2019

Rais wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), Wallace Karia mbali na kukemea tabia ya wanachama au viongozi wa soka nchini kwenda kinyume na katiba pamoja na kanuni za mpira wa miguu lakini alieleza mafanikio ya timu ya taifa ya soka la ufukweni.

Rais wa TFF Wallace Karia

Akiongea jijini Arusha kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa TFF, uliofanyika Jumamosi Februari 3, 2019, Karia alisema moja ya vitu vya kujivunia ni hatua kubwa ambayo taifa limepiga kwenye soka la ufukweni.

''Kwenye soka la ufukweni tumefanikiwa sana na sasa tupo kwenye 60 bora kidunia na Afrika tupo kwenye 10 bora'', alisema Karia.

Katika viwango vya ubora duniani, Tanzania ipo nafasi ya 58 huku Afrika ikiwa nafasi ya 8 ambapo Karia alisisitiza kuwa mipango iliyopo ni kuhakikisha inaingia kwenye 10 bora duniani kupitia kuifanyia maandalizi mazuri na kushinda vikombe itakavyoshiriki.

Mwishoni mwa mwaka 2018, timu hiyo ya taifa inayofundishwa na Boniface Pawasa, ilishiriki AFCON ya soka la ufukweni iliyofanyika Misri na kumaliza katika nafasi ya 6 kati ya timu 8.