Tuesday , 27th Nov , 2018

Mlinzi wa kushoto wa Manchester United Luke Shaw ameweka wazi kuwa inahitaji kuwa mstahimilivu ili kucheza kwenye kikosi cha Manchester United chini ya kocha Jose Mourinho.

Luke Shaw akiwa na Jose Mourinho

Shaw ameweka wazi hilo wakati akiongea kuelekea mchezo wa timu hiyo kwenye ligi ya mabingwa Ulaya kundi H, ambapo United inalazimika kushinda mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.

''Wachezaji wanahitaji 'ngozi imara' ili kucheza chini ya kocha Jose Mourinho, mara nyingi analalamika kuhusu sisi wachezaji wa kizazi hiki akijaribu kulinganisha na miaka iliyopita hivyo anataka tuoneshe kitu na kuitetea klabu'', amesema.

Mourinho alikaririwa baada ya suluhu dhidi ya Crystal Palace kwenye EPL wikiendi iliyopita akiwataka wachezaji kuonesha uwezo zaidi kitu ambacho siku za nyuma amewahi kumlalamikia Luke Shaw kwa kumwambia anatakiwa kubadilika ili apate nafasi kwenye kikosi chake.

Manchester United ipo katika nafasi ya 2 kwenye msimamo wa kundi H ikiwa na alama 7 nyuma ya Juventus yenye alama 9. United inakabiliana na Young Boys yenye alama 1 nafasi ya 4 huku Juventus wakikwaana na Valencia yenye alama 5 nafasi ya 3.