
Mechi za raundi ya 3 ya Kombe la FA, ambalo kwa sasa linaitwa Emirates FA Cup ambalo huzikutanisha klabu za ligi kuu na ligi daraja la kwanza nchini Uingereza, mechi zake zitachezwa mwishoni mwa wiki hii.
Arsenal ambao ndiyo Mabingwa watetezi baada ya kulitwaa Kombe hilo kwa mara ya pili mfululizo, Jumamosi watakuwa Emirates kucheza na Sunderland wakati mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Uingereza, Chelsea, Jumapili watakuwa kwao Stamford Bridge kucheza na timu ya daraja la chini inayoitwa Scunthorpe United.
Jumamosi Manchester United watakuwa Old Trafford kucheza na Sheffield United, na Manchester City watakuwa ugenini kucheza na Norwich City.
Liverpool wao watafungua dimba Ijumaa wakiwa ugenini kuivaa Exeter City huku Jumapili Tottenham wakiwavaa Leicester City ambao wako nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza.