Tuesday , 14th Mar , 2017

Beki wa kushoto wa Azam FC Gadiel Michael , amefurahishwa kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, kwa mechi mbili za kimataifa.

Gadiel Michael

Michael mwenye umri wa miaka 21,  ni kati ya nyota saba wa Azam FC walioitwa na mwalimu wa Stars, Salum Mayanga, alipotangaza wachezaji 26 watakaoingia kambini Machi 19 kujiandaa michezo ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Mara baada ya kuitwa kwa mara ya kwanza kikosi hicho, Gadiel alionesha kufurahishwa huku akimshukuru Kocha Mayanga kwa kutambua uwezo wake.

“Ninafuraha sana, nimechezea timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 huko nyuma, najisikia vizuri kuitwa kwenye kikosi cha wakubwa, namshukuru kocha kwa kutambua uwezo wangu, naahidi kama ninavyofanya Azam FC nitaendelea kupambana kwa ajili ya kupigania namba kikosini,” alisema Gadiel.

Wachezaji wa Azam FC walioitwa wako saba ambao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na Gadiel Michael, aliyeitwa kwa mara ya kwanza, viungo Himid Mao ‘Ninja’, pamoja na Frank Domayo ‘Chumvi’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambao wamerejeshwa kwenye kikosi hicho baada ya kukosekana kwa muda mrefu.

Kwa idadi hiyo ya wachezaji, inaifanya Azam FC kuwa miongoni mwa timu mbili zilizotoa wachezaji wengi katika kikosi hicho, ikilingana na Simba ambayo nayo imetoa wachezaji saba, huku kwa upande wa Yanga wakiitwa wanne pekee.