Wednesday , 13th Jul , 2016

Kikosi cha Mtibwa Sugar kimeendelea na mazoezi yake chini ya Kocha Salum Mayanga ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga

Mayanga amesema, anaendelea kukinoa kikosi chake ili kuhakikisha kinafanya vizuri na kuleta ushindani zaidi msimu ujao huku akiendelea kuangalia baadhi ya wachezaji wanaofanya majaribio na kikosi hicho kwa ajili ya kuongezea nguvu ndani ya kikosi cha Mtibwa ili kukiweka kikosi katika hali nzuri zaidi ya msimu uliopita.

Mayanga amesema, ili kuhakikisha anapata wachezaji watakaoziba pengo la wachezaji walioondoka katika klabu hiyo hivi sasa wameshaanza mazungumzo kwa baadhi ya wachezaji huku wakitoa nafasi kwa vijana ambao wanafanya majaribio kwa siku ya leo pekee na wataangalia wenye uwezo wa kuongeza nguvu katika klabu hiyo wataungana nao kwa ajili ya kuboresha kikosi zaidi.

Mayanga amesema, baada ya wiki moja anaamini atakuwa amepata kikosi kamili cha wachezaji ambao watafanya nao kazi ndani ya kikosi hicho ili kuleta ushindani zaidi ya msimu uliopita.

Mayanga amesema, siku zote anaamini Mtibwa Sugar ni timu bora na haijalishi mchezaji gani amekuja na mchezaji gani ameondoka hivyo kiuhalisia anaona timu imebaki na wachezaji wengi na kwa upande wake ataendelea na idadi kubwa ya wachezaji aliowakuta na kuongeza wachache kwasababu timu ilimaliza msimu uliopita kwenye ubora mzuri hivyo hana wasiwasi.

Mayanga amesema, soka ni biashara na inafika mahali vijana wanajengwa na inafika mahali pia wanataka kuondoka hivyo viongozi hawatakuwa na pingamizi iwapo wataondoka kwa kufuata taratibu za sheria na kanuni na timu ya Mtibwa Sugar itaendelea kusaidia kujenga vipaji vya vijana kwa ajili ya timu na Taifa kwa ujumla na kwakuwa uwezo wa kuandaa vijana upo na vijana wataendelea kuandaliwa.

Mayanga amesema, haoni tofauti kubwa kwa alipotoka na aliposasa kikubwa ni kufuata kanuni za kuongoza mpira kwa umakini zaidi.

Kikosi cha Mtibwa Sugar kinaendelea na mazoezi jijini Dar es salaam kwa takribani wiki sita huku kikisubiri msimu ujao wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara.

Mayanga aliyekuwa akikinoa kikosi cha wajelajela Tanzania Prisons ya jijini Mbeya msimu uliopita amesaini kukinoa kikosi cha Mtibwa kwa muda wa miaka miwili akichukua nafasi ya Mecky Maxime ambaye kwa sasa anaifundisha klabu ya Kagera Sugar.