Federer amefikia mafanikio hayo baada ya kumshinda Marin Čilić wa Croatia kwa seti 6-2 6-7 (5-7) 6-3 3-6 6-1 katika fainali iliyomalizika mchana huu jijini Melbourne Australia.
Nyota huyo raia wa Uswis mwenye miaka 36, amewafikia nyota wa tenisi Serena Williams wa Marekani, Margaret Court wa Australia na Steffi Graf wa Ujerumani ambao wameshinda mataji 20 ya Grand Slam kila mmoja.
Federer pia amewafikia Novak Djokovic na Roy Emerson ambao kila mmoja ametwaa mara sita ubingwa wa michuano ya wazi ya Australia kwa upande wa wanaume.
Baada ya kushinda mchezo huo wa fainali Federer amesema amefurahi sana na taji hilo limemwongezea nguvu ya kuendelea kusaka mafanikio zaidi licha ya umri wake kuanza kumtupa mkono.

