Sunday , 14th Feb , 2016

Wagosi wa kaya Coastal Union na beki wao kisiki wa pembeni aliyekatika timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba Miraji Adam wameweka rekodi nyingine kwa kuifunga timu ambayo ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo katika ligi kuu bara msimu huu Azam FC

Azam FC imeshindwa kuiengua kileleni mwa Ligi Kuu ya sokaTanzania Bara Simba SC, baada ya jioni ya leo kufungwa bao 1-0 na Coastal Union uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Shukrani zimuendee mfungaji wa bao hilo pekee, ambalo linavunja rekodi ya Azam FC kutofungwa msimu huu, beki wa kulia Miraj Adam aliyetikisa nyavu za Azam kunako dakika ya 67.

Adam aliyefunga pia katika ushindi wa 2-0 Coastal Union ikivunja rekodi ya Yanga SC kutofungwa msimu huu – leo alifunga kwa shuti la mpira wa adhabu pia, baada ya kuanzishiwa na beki mwenzake wa pembeni, Adeyum Saleh Ahmed.
 
Kipa Aishi Manula ana kila sababu ya kubeba lawama kwa bao hilo, kwani alidaka mpira na kulala nao kwa muda mrefu huku akiugulia maumivu badala ya kuutoa nje kwanza na mwamuzi Vincent Mlabu kutoka Morogoro aliyesaidiwa na Gasper Ketto na Mohammed Mkono akawaadhibu Azam.

Matokeo hayo yanaifanya Coastal Union ifikishe pointi 16 baada ya kucheza mechi 19 na kupanda hadi nafasi ya 13, kutoka ya 16 ilipokuwa inashikilia mkia, wakati Azam FC inabaki na pointi zake 42 za mechi 17, nyuma ya Yanga SC yenye pointi 43 za mechi 18 na Simba SC pointi 45 za mechi 19.

Mchezo huo wa Coastal Union na Azam FC umechezwa sambamba na mchezo uliopigwa Shinyanga katika dimba la Mwadui Complex ambako huko ilishuhudiwa wenyeji wachimba almas wa Mwadui wakibanwa mbavu na maafande wa magereza toka Mbeya timu ya Tanzania Prisons kwa kwenda suluhu ama bila bila 0-0 ama sare tasa.