Monday , 20th Jun , 2016

Timu ya Cleveland Cavaliers imekua timu ya kwanza kutwaa ubingwa NBA ikitokea nyuma kwa kipigo cha michezo mitatu kwa mmoja baada ya alfajiri ya leo kuwanyuka waliokua mabingwa watetezi Golden State Warriors vikapu 93-86.

LeBron James ameibuka shujaa wa mabingwa hao wapya wa NBA kwa kufunga vikapu 27, mipira 11 ya kunyakua na pia akatoa mipira 11 ya msaada huku Kylie Irving naye akiisaidia timu yake Cleveland Cavaliers ishinde taji kwa mara ya kwanza tangu miaka 52 iliyopita.

Mara baada ya mchezo kumalizika LeBron James alitajwa kuwa mchezaji bora wa ghali (MVP) kwa msimu huu na kubeba tuzo hiyo kwa mara ya tatu katika maisha yake ya kucheza mpira wa kikapu.

Akizungumza mara baada ya mchezo Lebron amesema alijiwekea lengo la kuleta heshima katika Jiji analoishi kama alivyoisaidia Miami Heat msimu wa 2012-2013 kufanya hivyo.

Kwa upande wa mchezaji bora wa NBA Steph Curry aliyefunga vikapu 26 amesema amejisikia vibaya kushuhudia wapinzani wao wakishangilia ubingwa ambao anadhania walipaswa wao kushinda.

Nyota huyo amesema hawana namna zaidi ya kuwapongeza wapinzani wao kwa kutwaa taji hilo msimu huu.