Monday , 12th Jan , 2015

Baraza la Michezo nchini BMT limesema litahakikisha linasimamia vyama vya michezo ili kuweza kuboresha michezo nchini kwa lengo la kuitangaza nchi katika ramani ya michezo.

Henry Lihaya, Katibu Mkuu BMT

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa BMT, Henry Lihaya amesema mwaka jana kulikuwa na uchaguzi katika vyama hivyo lakini baadhi ya vyama havikufanya uchaguzi huo kutokana na changamoto mbalimbali zilizovikumba vyama hivyo.

Lihaya amesema, uchaguzi ni sehemu ya utawala bora ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kukuza michezo hivyo watahakikisha wanasimamia vyama hivyo kwa mwaka huu ili kuweza kukamilisha uchaguzi na kuweza kupata viongozi watakaoweza kuongoza vyama hivyo na kuleta manufaa katika michezo.

Lihaya amesema, pamoja na uchaguzi katika vyama hivyo, lakini watajitahidi kuhakikisha wanaondoa migogoro iliyopo katika vyama ili kuweza kuboresha na kukuza michezo nchini, kwani migogoro katika vyama huchangia kwa asilimia kubwa kushusha kiwango cha michezo nchini.