Thursday , 14th Apr , 2016

Baraza la michezo nchini BMT limeitaka Klabu ya Yanga kuanza ndani ya siku saba kuanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake ili kuiweza kupata uongozi mpya utakaoiongoza klabu hiyo.

Kaimu katibu Mkuu wa BMT Mohamed Kiganja amesema, walishatoa maelekezo kwamba ndani ya siku saba wafanye utaratibu au wafanye uchaguzi kwani yote yanawezekana licha ya katiba yao kueleza kuwa uchaguzi ni ndani ya siku 60.

Kiganja amesema, Klabu hiyo inatakiwa kuanza kuchukua hatua kwa kila walichoambiwa kama ni kuanza mchakato wa uchaguzi lakini wawe wametimiza kwa muda walioambiwa.

Tayari barua ya kutakiwa kufanya uchaguzi imeshawafikia viongozi wa Yanga na wamekiri kuanza mchakato wa kuitisha uchaguzi hivi karibuni, Yanga inatakiwa kufanya uchaguzi kabla hawajarudiana na Al Ahly huko Cairo Misri.

Yanga sasa ipo chini ya uongozi ulioingia madarakani Julai 15 mwaka 2012 ambao uliingia mara baada ya kufanyika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu ambapo uongozi huo pia umemaliza muda wake.